Saturday, June 27, 2020

HOSPITALI YA MIREMBE YABORESHA UTOAJI WA HUDUMA ZA AFYA

HOSPITALI YA MIREMBE YABORESHA UTOAJI WA HUDUMA ZA AFYA.

Na, Mwandishi wetu

Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe imefanya mabadiliko katika utoaji wa huduma za matibabu kwa wagonjwa wa nje, ambapo muda wa kuanza kutoa matibabu ni saa moja asubuhi badala ya saa mbili asubuhi.

Lengo la uongozi wa hospitali kufanya mabadiliko hayo ni kuboresha huduma za afya ili kuwezesha watu mbalimbali kupata huduma za matibabu mapema zaidi na kwa wakati.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, Dkt. Paul Lawala amesema mabadiliko hayo yanahusu huduma zote za afya; ikiwamo huduma za afya ya akili pamoja na magonjwa ya mwili.Dkt. Isack Gesase wa Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe akimsikiliza mmoja wa wagonjwa waliofika kupatiwa Huduma ya matibabu hospitali hapo.

Dkt. Lawala amesema tangu kuanza kwa utekelezaji wa mabadiliko hayo  kumekuwapo na matokeo chanya kwa kuwa watumishi wamefurahia kuanza kutoa huduma mapema, huku wagonjwa na ndugu wakifurahia utaratibu mpya wa kupatiwa huduma mapema na kurejea nyumbani mapema.

“Matokeo chanya yameanza kuonekana kwani watumishi wameitikia wito wa kuwahi mapema na kuanza kutoa huduma saa moja asubuhi.

Hatua hii imesaidia watu mbalimbali kupata huduma za matibabu mapema na kwa wakati na pia watu wengi wamevutiwa na mabadiliko haya,” amesema Dkt. Lawala.

Naye Mkuu wa Kitengo Cha Wagonjwa wa Nje, Dkt. Isack Mrimi amewataka wananchi kufika katika  hospitali hiyo kupata huduma za matibabu kwa kuwa Mirembe ina wataalamu wabobezi wenye uwezo wa kutoa huduma bora na kwa wakati.

Huduma za afya katika Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe zinatolewa na wataalamu wetu ambao wako tayari kukuhudumia wakati wote.

Thursday, June 25, 2020

WAZAZI NA WALEZI MSIOGOPE KUTUMIA VIRUTUBISHI MCHANGANYIKO KWENYE VYAKULA VYA WATOTO WENU.

WAZAZI NA WALEZI MSIOGOPE KUTUMIA VIRUTUBISHI MCHANGANYIKO KWENYE VYAKULA VYA WATOTO WENU.

Na, Jackson Monela, TFNC

Wazazi na Walezi katika Wilaya za  Ikungi na Manyoni wametakiwa kuachana na imani potofu kuwa virutubisho mchanganyiko vina madhara kwa Watoto, na kuhofia kuvitumia, ilhali vimekuwa na msaada mkubwa katika kusaidia ukuaji mzuri wa mtoto na kusaidia katika kupambana na udumavu.

Wito huo umetolewa Mkoani Singida  na Mkurugenzi wa Elimu na Mafunzo ya Lishe  kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Bi.Sikitu Kihinga, wakati wa mafunzo kwa watoa huduma za afya  wa Halmashauri hizo, juu ya  matumizi ya Virutubisho mchanganyiko ambavyo hutolewa kwa Watoto wenye umri wa miezi 6 hadi 23.

Sikitu amesema Virutubisho mchanganyiko vina umuhimu mkubwa sana kwa watoto kwani vinasaidia kupambana na tatizo la udumavu, ikizingatiwa katika jamii  nyingi kumekuwa na changamoto baadhi ya wazazi na walezi kushindwa kuandaa mlo unaokidhi mahitaji yote ya virutubishi vinavyohitajika kwa mtoto.

Washiriki wa mafunzo ya matumizi ya virutubishi mchanganyiko wakiwa katika picha ya pamoja baada ya mafunzo hayo yalifanyika kuanzia tarehe 15 hadi 17 Juni 2020 katika halmashauri za IKungi na Manyoni mkoani SINGIDA.

Halmshauri za Ikungi na Manyoni zipo kwenye  utekelezaji wa mradi wa ugawaji virutubisho mchanganyiko kwa Watoto wenye umri wa miezi 6 hadi 23, ukiwa chini ya Ufadhili wa Shirika la Nutrition  International na kusimamiwa na Shirika la World Vision, ambapo mpaka kufikia mwezi Machi 2020 katika halmashauri hizo mbili jumla ya Watoto 16416 wamefikiwa na huduma hiyo

Saturday, May 23, 2020

SERIKALI YATOA RIPOTI YA UCHUNGUZI WA MAABARA YA TAIFA YA AFYA YA JAMII NA KUBAINI MAPUNGUFU MBALIMBALI

SERIKALI YATOA RIPOTI YA UCHUNGUZI WA MAABARA YA TAIFA YA AFYA YA JAMII NA KUBAINI MAPUNGUFU MBALIMBALI

Na WAMJW – Dar es Salaam

23/05/2020 

Serikali imetoa ripoti ya uchunguzi wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii iliyoko ofisi za Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binaadam (NIMR) jijini Dar es Salaam na kubaini mapungufu mbalimbali ya kiutendaji yaliyokuwepo katika maabara hiyo.

Akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo leo jijini Dar es Salaam, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mheshimiwa Ummy Mwalimu ametaja mapungufu yaliyobainishwa na kamati hiyo kuwa moja kati ya mashine za kupima sampuli za COVID-19 ilikuwa na hitilafu bila uongozi wa maabara kuchukua hatua za kuifanyia matengenezo.

Taarifa hiyo pia imebaini kuwepo kwa upungufu katika mfumo wa kimuundo, kiutendaji na uendeshaji wa kitaaluma katika upimaji wa vipimo, uhakiki wa ubora wa majibu na udhaifu katika uhifadhi wa vipimo vya COVID-19. 

Waziri Ummy amesema kamati hiyo pia imetaja kuwepo kwa upungufu wa wataalamu wenye sifa za mafunzo ya “Biotechnology & molecular Biology” katika sekta ya Afya ikiwemo katika Maabara Kuu ya Taifa.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu, akizungumza na waandishi wa Habari (Hawapo Pichani) kuhusu matokeo ya uchunguzi wa kamati iliyoundwa kuchunguza maabara ya Afya ya Jamii iliyopo NIMR jijini Dar es salaam, kufuatia kutoa majibu yenye mkanganyiko ya Vipimo vya ugonjwa Corona.


Kufuatia taarifa ya kamati ya uchunguzi wa Maabara ya Taifa kuhusu upimaji wa sampuli za ugonjwa wa COVID- 19, Wizara ya Afya imechukua hatua ya kuhamisha shughuli za upimaji wa COVID – 19 kutoka kwenye maabara iliyoko NIMR na  kuanza kutumika kwa mashine nyingine za maabara mpya iliyopo Mabibo, Dar es salaam.

“Kuanzia sasa shughuli zote za upimaji wa maabara ya taifa zitafanyika katika maabara mpya ya mabibo yenye vifaa vya kisasa vyenye ubora na uwezo wa kupima sampuli 1,800 ndani ya masaa 24” amesisitiza Waziri Ummy.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu, akizungumza na madereva wa malori yanayoenda nje ya nchi, namna ya kuchukuliwa vipimo vya maambukizi ya ugonjwa wa Corona, baada ya kufika katika maabara za afya ya jamii zilizopo Mabibo, kwa ajili ya kuchukuliwa vipimo.

Amesema maabara iliyokuwa inatumika awali na kukutwa na mapungufu ilikuwa na uwezo wa kupima sampuli 300 kwa masaa 24 na ilianzishwa mwaka 1968 katika ofisi za Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binaadam (NIMR), mtaa wa Obama kati kati ya jiji la Dar es Salaam zitaendelea kupima magonjwa mengine.
 
“hivi sasa Upimaji wa Sampuli zote za COVID-19 umehamishiwa kwenye Maabara hii ya Mabibo, Dar es Salaam ambayo kuanzia sasa ndiyo itakuwa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii. Maabara hii ambayo ujenzi wake umekamilika mwezi huu ina miundombinu inayojitosheleza, mashine za kisasa zinazoweza kupima sampuli nyingi na kutoa majibu ya uhakika na kwa haraka” amesema Waziri Ummy. 

Aidha, Wizara imeshaandaa wataalam zaidi wenye sifa na vigezo kwa ajili ya Maabara hiyo na imeanza kurekebisha mfumo wa utawala, utendaji na kitaaluma ndani ya Maabara ya Taifa
Jengo la Maabara mpya ya Afya ya Jamii iliyopo Mabibo jijini Dar es salaam, ambayo itatumika rasmi  kuchukua vipimo vya wahisiwa wa ugonjwa wa virusi vya Corona nchini.

Waziri Ummy Mwalimu aliunda Kamati ya wataalam iliyoanza kazi rasmi tarehe 6, Mei, 2020 ya kuchunguza mwenendo wa maabara ya taifa ya afya ya jamii ikiwa ni pamoja na kuangalia mfumo mzima wa ukusanyaji na upimaji wa sampuli za COVID – 19. 

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi ametoa mwongozo wa kusaidia jamii kushiriki katika ibada ya shukrani na sala ya Eid El Fitr kwa hali ya usalama ili kuepusha kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya corona.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Prof. Makubi amewataka  wananchi kuchukua tahadhari katika siku tatu ambazo nchi itaingia katika maombi maalum ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kupungua kwa maambukizi ya virusi ugonjwa wa Corona.

“ ni muhimu wananchi wakasherehekea salama kwa kuchukuwa  tahadhari kwani ugonjwa huo bado upo” Amesisitiza Mganga Mkuu wa Serikali.

Katika kufanikisha uwepo wa mazingira salama wakati wa shukrani na sala ,Viongozi wa Mitaa, Viongozi wa Afya na uongozi wa maeneo yote ya Ibada na misikitini wanapaswa kuhakikisha uwepo wa vifaa vya kunawia mikono, maji tiririka na sabuni au vitakasa mikono kwa ajili ya usafi binafsi wa waumini wote katika maeneo ya kuingilia .

Aidha, Prof. Makubi ameshauri sehemu za kufanyia ibada ziwe na nafasi ya viti kupangwa zaidi ya mita moja kwa wale wanaokaa au kusimama na wananchi wote wanapokwenda kushiriki au kutembelea maeneo ya Ibada/Sala wanashauriwa watumie barakoa za vitambaa ambazo kwa sasa zipo kwa wingi na zinatengenezwa hapa nchini na wananchi wenyewe.

Amewataka wananchi kuepuka mikusanyiko na kuhakikisha wanakaa umbali usipoungua mita moja kati ya mtu na mtu wakati wote wa shukrani na wakati wa shukrani waendesha ibada/sala wawakumbushe wananchi mara kwa mara kuzingatia taratibu za kujikinga na maambukizi kama inavyoelekezwa na wataalamu wa afya.

Mganga Mkuu wa Serikali amewakumbusha Wamiliki wa vyombo vya usafiri wa umma kuzingatia maagizo ya Serikali ya kutosimamisha abiria kwenye mabasi, na vilevile wahudumu wote wawe wamevaa barakoa za vitambaa.


Wednesday, May 20, 2020

SERIKALI INAHAKIKISHA WALENGWA WOTE WA CHANJO WANAFIKIWA KATIKA KIPINDI CHA CORONA

SERIKALI INAHAKIKISHA WALENGWA WOTE WA CHANJO WANAFIKIWA KATIKA KIPINDI CHA CORONA

Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia Mpango wa Taifa wa Chanjo imejipanga kuwafikia walengwa wote waliostahili kupata chanjo na kuhakikisha kiwango kinabaki vilevile kama ilivyotarajiwa.

Hayo yamesemwa na Ofisa Mradi kutoka Mpango huo Lotalis Gadau wakati wa usimamizi elekezi wa kukagua utoaji huduma za chanjo  katika Mkoa wa Pwani  kwa kushirikiana na Engender Health kupitia Merck Sharp& Dohme B.V (MSD).

Gadau alisema kuwa katika kipindi hiki cha nchi kukabiliana na Ugonjwa wa Corona, Wizara imejipanga kuhakikisha watoa huduma wa afya wanaendelea kutoa huduma za chanjo kwa watoto wadogo pamoja na wasichana ambao walikua wapate chanjo ya kujikinga na saratani ya mlango wa kizazi(HPV).

“Kama Wizara tumejipanga vizuri kwa kuhakikisha chanjo zote zinakuwepo kwa wakati kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na kuhakikisha watoto wote waliokuwa wanatarajia kupata chanjo wanapata,na watoa huduma wanachukua tahadhari zote za kujikinga na ugonjwa huu”,

Alisema walikuwa wakisikia wananchi wana wasiwasi kufika kwenye vituo vya kutolea huduma,“tumepita kwenye vituo vya afya kwenye mkoa huu na tumeona hali ni nzuri kwani wazazi na mabinti wengi wanakuja kwenye vituo na tumewasisitiza kila mmoja anayeenda awe balozi anaporudi nyumbani kuhakikisha wataambiana ili kila anayestahili kupata chanjo anaenda kwenye kituo cha afya chochote cha jirani aweze kupata chanjo”.

Vile vile alisema kuhusu mabinti ambao waliokua wapate  chanjo ya kuzuia  saratani ya malango wa kizazi  tofauti na awali ambapo walikua wakifuatwa mashuleni inasisitizwa wafike kwenye  vituo cha kutolea huduma za afya  vya karibu waweze kupata chanjo hiyo.

 Upande wa watoto wadogo, Bi. Gadau amesema hivi sasa umewekwa utaratibu kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka miwili ambao wanastahili kupatiwa chanjo wao wanatakiwa kupata chanjo kama ilivyo kawaida”Kwa kipindi hiki watoto ambao wamekamilisha ratiba ya chanjo na wanafika kituoni kwa ajili ya uzito tu wao wanatakiwa waende kila baada ya miezi mitatu hii ni kuepuka misongamano na tunasisitiza elimu ya afya ambayo ilikua ikitolewa kwa muda mrefu au kusubiriana kwa sasa  itatolewa kwa muda mfupi usiopungua dakika tano lakini endapo mtoto atapata homa au tatizo lolote anatakiwa kupekekwa kwenye kituo cha afya kwa ajili ya matitabu.

Naye Mratibu Huduma za Chanjo kwa Mkoa wa Pwani Abbas Hincha amesema kuwa asilimia 90 ya walengwa wa chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi kwa mabinti wenye umri wa miaka 14 ambao hapo awali walikuwa wakipatiwa wakiwa shuleni ila kutokana na janga hili wanashirikia na walimu wa shule zao kwani walikua wameandikishwa hivyo wanawapatia namba za simu na kuwapigia wazazi na walezi ili kuwapeleka kupatiwa chanjo hiyo.

Alisema katika mkoa wake wamepanga mikakati mbalimbali ikiwemo ya kuwashirikisha  watoa huduma ngazi ya jamii kuwatafuta mabinti hao kwenye maeneo yao na kuwakumbusha kwenda kupata chanjo.

Alisema muamko kwa chanjo kwa upande wa watoto wadogo unaendelea vizuri na kuna muitikio mzuri hivyo wanaendela kutoa elimu jinsi ya kujikinga na Corona na kwenye vituo ambavyo havina nafasi kubwa wanatoa huduma hizo nje ya kituo ili kuzingatia umbali wa mita moja kati ya mtu na mtu

 

HOSPITALI YA MIREMBE YABORESHA UTOAJI WA HUDUMA ZA AFYA

HOSPITALI YA MIREMBE YABORESHA UTOAJI WA HUDUMA ZA AFYA. Na, Mwandishi wetu Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe imefanya mabad...