FEDHA ZA WADAU WA MAENDELEO ZITUMIKE KUTATUA CHANGAMOTO ZA WANANCHI.

Na. WAF, Dar Es Salaam

Watalamu wa Afya nchini, wametakiwa kuwa wazalendo katika kusimamia fedha zinazotolewa na  wadau wa maendeleo, ili kuhakikisha wanatatua  changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi kama ilivyo adhma ya Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. 

Wito huo  umetolea Jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Afya Dkt.Godwin Mollel  mara baada ya kufunga  kikao kazi cha tathmini ya namna Tanzania ilivyoweza kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa UVIKO-19.

Dkt. Mollel amebainisha  kuwa  wadau wengi wamekuwa wakileta fedha nyingi kwenye sekta ya afya, lakini fedha hizo zimekuwa hazitumiki ipasavyo katika kusaidia sekta hiyo, huku nyingine zikiishia kutumika katika semina na makongamano na kupelekea kushindwa kuwanufaisha wananchi ambao ndiyo walengwa. 

“Zinakuja fedha nyingi kutoka kwa wadau, lakini tukishuka chini katika ngazi ya msingi hatuoni matokeo chanya, tuige mfano wa Mhe. Rais  Dkt. Samia Suluhu Hassan namna alivyotumia fedha za COVID katika kuboresha huduma za afya nchini mfano katika ngazi ya msingi kumejengwa majengo ya dharura na majengo ya wagonjwa maututi.” Amesisitiza Dkt. Mollel.

Akizungumzia kuhusu zoezi la tathmini baada ya kukabiliana na mlipuko wa UVIKO-19 Dkt. Mollel amesema yapo mengi ya kuzungumzia katika tathmini hiyo, hivyo ni jukumu la wataalamu na wadau walioshiriki kwenye kikao hicho kuhakikisha tathimini yao inakuja na matokeo chanya ya kuleta tija kwa wananchi.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Dharura na Maafa Wizara ya Afya, Dkt. Angela Samwel amesema mapendekezo yote yaliyotolewa na watalaamu pamoja na  wadau walioshiriki kwenye tathmini hiyo yatachukuliwa kama sehemu ya kupokea masuala yote mazuri na kuboresha mapungufu yaliyojitokeza wakati wa kukabiliana na mlipuko wa UVIKO-19

Dk. Angela ameongeza kuwa Tathmini ya namna nchi ilivyokabiliana na mlipuko wa UVIKO 19 imehusisha wadau mbalimbali kutoka Wizara mbalimbali ikiwemo, Taasisi za Serikali, Hospital za Taifa, Hospital binafsi, Waganga wakuu wa mikoa,wadau wengine kutoka Mashirika ya  Umoja wa Mataifa na Wadau wengine wa Maendeleo.

MWISHO:

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MATOKEO YA UTAFITI WA HALI YA LISHE YA WANAFUNZI SHULE YA MSINGI YATOLEWA

TFNC YAIBUKA MSHINDI WA JUMLA MAONESHO YA SIKU YA CHAKULA DUNIANI.

WANAFUNZI WANYWE MAZIWA SHULENI-UMMY MWALIMU.