WEKENI KIPAUMBELE KWENYE UTEKELEZAJI WA AFUA ZA LISHE.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI imetoa wito kwa Serikali kuendelea kuweka kipaumbele katika utekelezaji wa afua mbalimbali za lishe nchini, ili kuwezesha kuwa taifa lenye watu wenye afya na lishe bora na kuweza kufikia malengo endelevu.

Wito huo umetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Mhe. Stanslaus Nyongo (MB) baada ya kufanya ziara katika Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania ili kujifunza na kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na Taasisi hiyo.

Mhe.Nyongo amesema afua za lishe zinahitaji kuwa na uwekezaji wa kutosha na kupewa kipaumbele, kwani usipowekeza kwenye lishe unaweza kujikuta unatibu wananchi wengi kwa sababu ya lishe mbovu, wakati unaweza kutumia lishe kama tiba namba moja na yenye gharama nafuu.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIWMI wakipata maelezo kutoka kwa wataalamu wa Maabara ya Chakula na Lishe Tanzania iliyopo Mikocheni, ikiwa ni ziara ya kujifunza na kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na Taasisi hiyo. Ziara hiyo imefanyika Septemba 12, 2023 jijini Dar es Salaam.

“Waheshimiwa wabunge wenzangu hili halina mjadala   twendeni tukaishauri Serikali tuhakikishe wanaweka kipaumbele kwenye afua za lishe, utaendelea kutibu wananchi wengi kwa sababu ya lishe mbovu wakati lishe ni tiba namba moja tena ya bei nafuu.”Amesema Mhe. Nyongo. 

Aidha Mhe. Nyogo amesisitiza elimu ya lishe iendelee kutolewa zaidi kwa jamii ya Watanzania, ikihusisha makundi yote muhimu, kwani bado kuna upotoshaji mkubwa unaofanyika kwenye masuala ya lishe, na wapo baadhi ya watu  wanaibuka na bidhaa mbalimbali za lishe, ambazo zimekuwa na matokeo hasi kwa watumiaji na nyingine kuwaletea shida kiafya watumiaji hao.

“lazima tutoe ushauri ni chakula gani watu waweze kutumia, maana sasa hivi lishe imevamiwa kila moja ameibuka na lake, sasa kila mtu ni mtaalamu wa lishe.” Amesema Mhe. Nyongo.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema wataendelea kuimarisha eneo la lishe kutokana na kuwa ni la msingi kwa taifa, na maeneo yenye shida kwa upande wa utekelezaji wa afua mbalimbali za lishe  tayari yameonekana na Wizara kwa kushirikiana na Taasisi ya Chakula na Lishe itachukua hatua za kuboresha zaidi.

Hata hivyo Dkt. Mollel ameiomba kamati ya Bunge kuangalia namna ya kuweza kuipatia nguvu Taasisi hivyo, kwani bado haina misuli ya kuweza kudhibiti baadhi ya masuala yanavyoibuka kila kukicha kuhusiana na masuala ya Chakula na Lishe.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi ya Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Bw. Obbey Assery, ameiomba kamati ya kudumu ya Afya na Masuala ya UKIMWI kuwa sehemu ya kuisemea lishe katika ngazi ya Chini hadi Taifa, na kuiomba kupigia  kelele suala la kutenga shilingi 1000 za afua za lishe kwa ajili ya watoto chini ya umri wa miaka 5 ili zitumike katika utekelezaji wa afua mbalimbali za lishe

 

MWISHO:

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MATOKEO YA UTAFITI WA HALI YA LISHE YA WANAFUNZI SHULE YA MSINGI YATOLEWA

TFNC YAIBUKA MSHINDI WA JUMLA MAONESHO YA SIKU YA CHAKULA DUNIANI.

WANAFUNZI WANYWE MAZIWA SHULENI-UMMY MWALIMU.