MATOKEO YA UTAFITI WA HALI YA LISHE YA WANAFUNZI SHULE YA MSINGI YATOLEWA

Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania kwa kushirikiana na Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria imetoa matokeo ya utafiti wa hali ya lishe ya wanafunzi wa Shule za Msingi uliofanyika mwaka 2021 na kuhusisha mikoa 26 ya Tanzania bara.

Utafiti huo ulihusisha shule za umma 650 na wanafunzi 64,465 ulilenga kutathimi kiwango cha Maambukizi ya Malaria na Utapiamlo miongoni wa wanafunzi, ambapo katika viashiria vya lishe, utafiti huo umebaini wanafunzi waliopo katika shule za msingi bado wana changamoto nyingi za kilishe zinazowakabili.

Akiwasilisha taarifa za utafiti huo kwa wadau mbalimbali wa lishe kutoka Idara za Serikali, Mashirika ya Kimataifa, wadau wa maendeleo, asasi za kiraia na wadau wengine, Afisa Lishe Mtafiti kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt.Geofrey Mchau, amesema wameweza kubaini wanafunzi wengi bado wana lishe duni, uzito uliopungua, uzito uliokithiri na upungufu wa damu kwa kiwango kikubwa.


Dkt. Mchau amesema utafiti huo umebaini pia mazingira mengi yanayozunguka shule hizo yanashawishi wanafunzi wengi kuwa na ulaji wa chakula ambacho si sahihi, kutokana na shule nyingi kuzungukwa na maduka, na vibanda vya wauzaji wadogo wadogo wa vyakula ambavyo si rafiki kwa afya za wanafunzi.

Akizungumzia juu ya tatizo la Upungufu wa damu kwa wanafunzi hao Dkt. Mchau amesema Utafiti huo umeonyesha asilimia 32% ya watoto wanaoenda shuleni wana tatizo la upungufu wa damu kwa kiwango kikubwa na maeneo ya ukanda wa bahari (Mikoa ya Pwani) na ile iliyopo kwenye ukanda wa ziwa Victoria ndiyo imeonekana kuwa na changamoto kubwa ya watoto upungufu wa damu

Dkt Mchau amesema tatizo jingine ambalo limeonekana kuwaathiri wanafunzi hao ni tatizo l;a uzito uliokithiri ambao wenyewe umebainika kuwa asilimia 3.8 huku ukondefu ukiwa ni asilimia 2.6.


Akizungumza wakati wa kufungua kikao cha kupokea taarifa hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt. Germana Leyna amesema kuna haja ya kukusanya nguvu na kuweka rasilimali zaidi katika utekelezaji wa afua mbalimbali kwa kuzingatia mifumo rasmi ya kiutawala, kiutendaji, mila na desturi za maeneo husika.

Dkt.Germana amesema zifanyike tafiti nyingi zaidi zinazolenga kundi hili ambalo ni muhimu kwa maendeleo ya taifa na taarifa hizi ni budi zikaendelea kufanyiwa uchambuzi ili kupata maeneo yanayoweza kuleta matokeo ya haraka kuendana na kasi ya Serikali katika kuimarisha sekta ya Elimu na Afya.

Kwa upande wake mwakilishi wa shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) anayeshughulikia Lishe Bi Vera Kwara ambao wamefanikisha kufanyika kwa Utafiti huo, amesema taarifa zilizopatikana katika utafiti huo zitasaidia utekelezaji wa sera na hatua za haraka zinazoweza kutumika katika kuboresha hali ya lishe nchini.



Utafiti wa hali ya lishe ya wanafunzi shule ya Msingi uwa unafanyika kila baada ya miaka miwili, na ripoti hii ni mahsusi kwa sababu taarifa za wanafunzi hawa hazikusanywi kwenye tafiti nyingine kama za TDHS na ile ya TNNS, hivyo taarifa zinazopatika kwenye utafiti huu ni muhimu kwani huweza kutumika kutengeneza mipango inayoweza kutumika kutatua changamoto mbalimbali za kilishe.


Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

TFNC YAIBUKA MSHINDI WA JUMLA MAONESHO YA SIKU YA CHAKULA DUNIANI.

WANAFUNZI WANYWE MAZIWA SHULENI-UMMY MWALIMU.