WADAU WA AFYA WAKUBALIANA KUANZISHA BENKI YA MAZIWA YA MAMA TANZANIA
Na, MwandishiWetu
Wadau wa Afya na Lishe nchini wamekutana na kufanya kikao kazi cha pamoja kujadili namna ya kuanzisha Benki ya Maziwa ya Mama, lengo likiwa kuboresha hali ya afya na lishe za watoto wachanga hususani wanaozaliwa na uzito pungufu, wagonjwa sana, ambao hawana mama au mama zao ni wagonjwa mahututi na hivyo kukosa maziwa ya mama jambo linalosababisha athari kwa watoto kiafya na kuongeza vifo vya vichanga hivyo.
Akizungumza
wakati wa kufungua kikao kazi hicho, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi kitengo cha
Lishe Wizara ya Afya, Neema Joshua amesema kuwa Wizara ya Afya inaunga mkono
jambo hilo na ipo tayari kushirikiana na wadau kuhakikisha linakamilika kwa
wakati.
“Niwapongeze wadau walioanzisha harakati hizi
za kuanzisha Benki ya Maziwa ya Mama hapa Nchini kwa lengo la kuboresha hali ya
afya na lishe za watoto wetu hususani wanaozaliwa na uzito pungufu au kabla ya
wakati na mama zao kukosa maziwa ya kutosha jambo linalosababisha watoto hao
kutokuwa vizuri” Amesema Neema Joshua.
Kwa
upande wake Daktari wa Watoto kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila,
Dkt. Lucy Mpayo amesema, Benki ya Maziwa ya mama ni huduma inayowawezesha akina
mama kupata maziwa ya ziada, ambayo huchangiwa na wamama wengine kwa hiari na
kuhifadhiwa kwa usalama kisha kupatiwa watoto wenye mahitaji. Uwepo wa benki ya
maziwa kutawezesha watoto hao kupata
maziwa ya mama kwa muda muafaka na kusaidia kuimarisha afya zao, hususani
kuongezeka uzito kwa haraka Zaidi.
Daktari
wa Watoto kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Dkt. Lucy Mpayo
akiwasilisha mada wakati wa kikao cha wadau wa afya na lishe kilichofanyika
katika ukumbi wa mikutano hospitali ya Aga Khan, Dar es salaam.
Dkt.
Lucy Mpayo aliendelea kuhimiza kuwa mtoto aliyezaliwa na uzito pungufu akiwahi
kupewa maziwa ya mama katika siku za mwanzo baada za kuzaliwa humsaidia mtoto
katika kumkinga dhidi ya maradhi na kumuwezesha kukua vizuri na hivyo kumpunguzia
siku za kukaa hospitalini.
Aidha
Dokta Lucy amesema kuwa Hosptali ya Taifa Muhimbili Mloganzila ilifanya utafiti
wa mwaka mmoja kutoka Mei 2018 hadi Mei 2019 uliobaini kuwa asilimia 53 ya
watoto waliozaliwa na uzito pungufu chini ya kilo moja na nusu huchelewa
kuanzishiwa kupewa maziwa ya mama kwa zaidi ya siku mbili kutokana na sababu
mbalimbali ikiwemo mama kuwa mgonjwa baada ya kujifungua, kutokuwa na maziwa ya
kutosha pamoja na mtoto kuwa mgonjwa.
Uanzishwaji
wa Benki ya Maziwa ya Mama ulianza rasmi mwaka 1909 nchini Austria na kufuatiwa
na Amerika ya Kaskazini mwaka 1919 na kisha kuenea katika nchini nyingine.
Mwaka 1980 Benki nyingi za Maziwa ya Mama zilifungwa kutokana na hofu ya
maambukizi ya Virusi vya Ukimwi, lakini baada ya mikakati mingi kuanzishwa ya
kuzuia maambukizi ya vijidudu vya Virusi kwa kuwafanyia vipimo akina mama
wanaochangia maziwa yao na kisha kuyahifadhi maziwa hayo kwa usalama zaidi
benki hizo zilifungiliwa tena. Benki ya kwanza ya maziwa kuanzishwa Afrika ilikuwa Afrika Kusini
iliyoanzishwa mwaka 1980, na kisha kufuatiwa na Cape Verde 2011. Kwa upande wa
nchi za Afika Mashariki Kenya ndio nchi ya kwanza kuanzisha Benki ya Maziwa ya
Mama mwaka 2019.
Maoni
Chapisha Maoni