TFNC YATOA MAFUNZO KWA WAUGUZI NA WAKUNGA
Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania imeendesha kozi fupi kwa
wauguzi na wakunga, juu ya kumsaidia mama
kunyonyesha kwa usahihi kwa lengo la kuwajengea uwezo zaidi na kufanikisha
utoaji wa huduma bora zitakazosaidia kutokomeza utapiamlo kwa watoto.
Akizungumza wakati wa kugawa vyeti kwa wahitimu wa kozi hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania, Dkt. Germana Leyna amesema, mafunzo hayo yatawasaidia wahitimu kuongeza ufanisi katika maeneo yao ya kazi na kutoa huduma bora kwa wanawake wanaojifungua na kunyonyesha jambo litakalosaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha hali ya lishe za watoto wa kitanzania.
“Mafunzo haya yametolewa kwa njia
ya majadiliano kati ya washiriki na wawezeshaji, jambo litakalosaidia Taasisi
kubaini changamoto zinazowakabili kina mama kushindwa kunyonyesha ipasavyo na
hivyo kuwafundisha wauguzi na wakunga namna bora za kutatua changamoto hizo na
hatimaye kumwezesha mama kunyonyesha kwa usahihi” Amesema Dkt. Leyna.
Aidha Dkt. Leyna amewaomba wahitimu wa kozi hiyo kuwa mabalozi wazuri kwa kuboresha utendaji wao wa kazi na kuwahamasisha wengine kuja kusoma kozi hiyo pindi itakapotangazwa tena.
Awali wakati akimkaribisha
Mkurugenzi Mtendaji kufunga mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na
Mafunzo ya Lishe, Dkt. Esther Nkuba amesema kuwa wauguzi na wakunga ni watu
muhimu sana katika kufanikisha suala la unyonyeshaji katika jamii.
“Takwimu za mwaka 2022 za TDHS
zinatuonesha kuwa watoto wanaoanzishiwa kunyonyesha maziwa ya mama ndani ya saa
moja ni baada ya kuzaliwa ni asilimia 70, na watoto wanaopewa maziwa ya mama
pekee katika miezi sita ya mwanzo ni asilimia 64, lengo letu ni kufika asilimia
100, na hili linawezekana ndio maana tumeanza kutoa mafunzo haya kwa wauguzi na
wakunga kwa sababu ni watu muhimu sana katika kufanikisha unyonyeshaji katika
jamii” Amesema Dkt. Nkuba.
Kwa upande wake Mratibu wa
Mafunzo hayo Eliasaph Mwana amesema kuwa kozi hii imetolewa kwa siku nne
kuanzia tarehe 23/05/2023 hadi tarehe 26/05/2023 ambapo jumla ya watu watano
waliweza kushiriki na kuhitimu mafunzo hayo.
“Jumla ya watu 30 walifanya
maombi ya kusoma kozi hii lakini walioweza kujiunga na kuhudhuria ni watu
watano tu, hivyo tutafanya tathimini kubaini ni changamoto gani zilizosababisha
wau wengi kushidwa kuhudhuria ili tutakapotangaza tena kozi hii watu wengi
waweze kuhudhuria” amesema Mwana.
Naye Mkunga kutoa Halmashauri ya
Wilaya ya Bahi, Anitha Mganga ambeaye amehudhuria mafunzo hayo ametoa rai kwa
TFNC kuangalia ni kwa namna gani wataweza kutoa mafunzo haya mikoani ili
kuhakikisha elimu hii inawafikia watu wengi zaidi.
Maoni
Chapisha Maoni