MATUMIZI YA TOGWA KWA WATOTO
Togwa ni kinywaji baridi chenye ladha ya sukari na uchachu, ladha hiyo hutokana na utengenezaji wake; kwani togwa hutengenezwa kwa uji uliochachushwa. Togwa hutumiwa na watu wa rika tofauti (mtoto na mtu mzima).
Mkurugenzi wa Sayansi ya Chakula na Lishe kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt. Elifatio Towo anasema Togwa inayopendekezwa hapa ni ile ambayo haina kilevi “alcohol” uthibitisho wa kimaabara unaonesha kuwa togwa isiyokuwa na kilevi humpatia mtoto virutubishi vingi na humkinga dhidi ya magonjwa ya kuhara. Pia kwa mtoto anayeharisha akipatiwa togwa humsaidia kumrudishia maji mwilini mwake, yaliyopotea kutokana na kuharisha.
Dkt. Towo anasema Togwa huweza kudumu kwa muda mrefu bila kuharibika, hivyo humpunguzia kazi mzazi au mlezi wa kumuandalia mtoto togwa mara kwa mara.
Jinsi ya kutayarisha Togwa kwa ajili ya mtoto
· - Pika uji mzito kwa kutumia unga wa kawaida (mfano unga wa mahindi au muhogo);
· -Uji ukiiva, epua, acha upoe mpaka uwe vuguvugu;
· -Ongeza unga wa kimea kiasi kikombe kimoja cha chai kwenye uji uliojaa lita tano;
· -Koroga uji mpaka kimea kichanganyike vizuri na uji kuwa majimaji;
· -Funika na acha togwa ichachuke usiku kucha;
· -Baada ya hapo togwa itakuwa tayari kunywewa na ni salama kwa mtoto.
Muhimu:
Dkt Elifatio Towo anasema mtoto anayeshauriwa kupewa togwa ni yule aliyefikisha umri wa kuanza kupewa chakula cha nyongeza (mwenye umri kuanzia miezi 6), chini ya miezi sita aruhusiwi kupewa chakula na kinywaji chochote zaidi ya maziwa ya mama pekee. Mtoto anayepewa togwa aendelee kunyonyeshwa maziwa ya mama kila anapohitaji. Pamoja na togwa vyakula vingine ni muhimu kwa afya na makuzi ya mtoto.
Imeandikwa na Jackson Monela
Afisa Uhusiano wa Umma Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania
Maoni
Chapisha Maoni