WAZIRI MHAGAMA AIASA JAMII KUTOPUUZA VYAKULA VYA ASILI
WAZIRI MHAGAMA AIASA JAMII KUTOPUUZA VYAKULA VYA ASILI.
NA.MWANDISHI WETU
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye
Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama ameiasa jamii kuendelea kutumia vyakula vya asili
ili kuwa na afya bora na kuondokana na magonjwa yatokanayo na lishe duni.
Ameyasema hayo wakati wa ziara yake
ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mradi wa Lishe unaoratibiwa na Idara ya
Sera na Uratibu wa Shughuli za Serikali chini ya ofisi yake kwa kushirikiana na
wadau mbalimbali wa masuala ya lishe. Ziara hiyo iliyofanyika tarehe 20 Agosti,
2020 katika Halmashari ya Wilaya ya Songea pamoja na kutembelea zahanati ya
Likarangilo iliyopo Wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma katika kuadhimisha siku ya
lishe kijijini hapo.
Waziri Mhagama amesema kuwa, uwepo
wa vyakula vya asili ni muhimu sana katika jamii zetu kwa kuzingatia vina
virutubishi muhimu vya kuimarisha afya kwani hupatikana katika mazingira
yanayozunguka na ni vyakula visivyo na madhara kwa wengi.
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na
Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akimpima uzito mmoja wa watoto
waliohudhuria katika maadhimisho ya siku ya lishe katika kijiji cha Likarangilo
kilichopo Wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma, wakati wa kukagua utekelezaji wa afua
za lishe katika mkoa huo.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Alieleza uwepo wa lishe bora
unachangia kuchagiza maendeleo kwa jamii zetu kwa kuzingatia kuwa kila kundi
linahitaji kula chakula bora katika kuhakikisha afya zinaimarika ili kushiriki
katika shughuli za maendeleo.
“Makundi yote ikiwemo, watoto,
vijana na wazee yanahitaji kula mlo kamili na kwa wakati kwani changamoto za
ukosefu wa lishe bora husababisha kudhorotesha shughuli za maendeleo,”
Waziri aliongezea kuwa,
miongoni mwa changamoto zinakabili utekelezaji wa masuala ya lishe nchini ni
mitazamo hasi juu ya baadhi ya vyakula na kuona vimepitwa na wakati pamoja na
ukosefu wa elimu ya afya kwa wanajamii na kuona masuala hayo ni ya
makundi na matabaka Fulani.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akiuliza jambo kwa Afisa Lishe Mkoa wa Songea Bi. Anna Nombo (mwenye koti na sketi nyeusi) kuhusu uji lishe maalum kwa watoto wakati wa zoezi la kuhudumia watoto kwa vitendo kwa kuwapatia uji wenye lishe wakati wa kusherehekea siku ya lishe katika kijiji cha Likarangilo kilichopo Wilaya ya Madaba, Songea (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
“Tupambane kuhakikisha kila
mwananchi anawajibika katika kubadili mtazamo juu ya utumiaji wa vyakula vya
asili na kuondokana na hali ya kubeza vyakula hivyo na hii ianze na mtu
binafsi, familia, jamii kisha taifa kwa ujumla, “alisema Waziri Mhagama
Waziri aliiasa jamii kuwa na bidii
na kuendelea kudumisha desturi zililopo katika jamii na kuwakumbusha kushiriki
katika shughuli za kilimo na ufugaji wa wanyama, ndege, samaki ili kujipatia
vyakula vitokanavyo na uzalishaji huo.
“Ni muhimu kudumisha mila na
desturi zetu kwa kuhakikisha tunakula vyakula vya asili na tuondokane na
vyakula vya kisasa vyenye kutumia kemikali nyingi, hebu tuanze kula vyakula
vyetu vya asili ikiwemo wadudu na vyakula vya mbogamboga vinavyopatikana katika
jamii zetu kwa mfano hapa Songea kuna viyenje, senene, mangatungu, liderere,
kisamvu, nyeng’enya, chikandi, uyoga, mahungu, pulika na simbilisi tuvitumie
bila kuvipuuza, ”alisema Waziri Mhagama
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya
Songea Mhe. Pilolet Kamando alieleza furaha yake kwa kutembelewa na Waziri, na
kuendelea kuahidi kushughulikia maelekezo na maagizo ya kuhakikisha elimu ya
masuala ya afua za lishe yanatolewa kwa jamii ili kuondokana na changamoto ya
udumavu kwa watoto na magonjwa mengine yatokanayo na ukosefu wa lishe bora.
Alieleza pia Mkoa umeendelea
kupambana na masuala ya lishe kwa kutoa elimu kwa Watendaji wa Vijiji, Kata na
wahudumu wa afya, kuhakikisha elimu ya kubadili tabia inatolewa ili jamii iwe
katika hali nzuri katika masuala ya lisha.
“kumekuwa na mikakati mingi ya
kuhakikisha jamii zinaendelea kula vyakula vyenye tija, na hili lipo ndani ya
uwezo wetu na tutaendelea kuvitumia vyombo vya habari kwa kuhakikisha masuala
ya lishe yanakuwa ni ajenda ya kila siku,”alisema Mhe. Kamando.
Aliongeea kuwa, Mkoa umeendelea
kusimamia na kutenga bajeti ya kusaidia usimamizi wa afua za lishe na hii
imesaidia kupiga hatua na kupungua kwa hali ya udumavu kutoka asilimia 44 hadi
41.
Maoni
Chapisha Maoni