Jumapili, 9 Agosti 2020

WANAFUNZI WANYWE MAZIWA SHULENI-UMMY MWALIMU.

 WANAFUNZI WANYWE MAZIWA SHULENI-UMMY MWALIMU.

NA, TFNC DODOMA.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema atamwandikia barua Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako kutoa pendekezo kuanzia Septemba Mosi Mwaka huu, Kila shule ya Msingi na Sekondari iwe na kibanda cha maziwa kwa ajili ya wanafunzi kupata lishe.

Kauli hiyo aliitoa Jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa siku ya Lishe Kitaifa ambayo kwa mara ya kwanza maadhmisho ya siku hiyo yanafanyika nchini yakiratibiwa na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na wadau wengine wa Lishe nchini.

Waziri Ummy alisema kuanzisha vibanda vya maziwa shuleni hasa shule za kutwa, kutasaidia wanafunzi kuboresha afya zao, lakini pia kutasaidia kupanua soko kwa bidhaa hiyo muhimu.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu, pamoja na Naibu katibu Mkuu TAMISEMI (Afya) Dk. Doroth Gwajima (Mwenye skafu) wakisikiliza maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Kuzalisha maziwa ya Kwanzaa kutoka jijini Mwanza, akieleza namna walivyoweza kuongeza viritubishi vya viazi lishe na Mwani kwenye maziwa, ili kuongeza kwa wingi upatikanaji wa Vitamini A kwenye maziwa hayo wakati wa uzinduzi wa siku ya Lishe nchini ambayo Kitaifa ilifanyika jijini Dodoma.

Alisema utafiti wa Shirika la Afya Duniani (WHO) unaonesha kwamba kila mtu anatakiwa kunywa nusu lita ya maziwa sawa na lita 180 kwa mwaka lakini kwa sasa kila mtu anakunywa lita 40 kwa mwaka sawa na vijiko 10 vya chai kwa siku.

Waziri Ummy Mwalimu ameitaka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania kuharakisha Mwongozo sahihi wa uandaaji vyakula vya nyongeza kwa Watoto vyenye virutubishi ambao unaandaliwa na Taasi hiyo kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kupitia ufadhili wa shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP)

“Tukiwa na jamii yenye lishe bora ni Dhahiri tutakuwa tumefanikiwa kupambana na maradhi, ujinga,na umaskini na hatimaye taifa letu kuwa nchi ya uchumi wa viwanda kama ilivyodhaminiwa na Serikali ya Awamu ya Tano”Alisema Ummy Mwalimu

Awali akitoa neno la ukaribisho katika maadhimisho ya siku hiyo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt. Germana Leyna alisema wamekuja na siku hiyo, ambayo kwa mara ya kwanza inafanyika nchini lengo likiwa kuongeza uelewa juu ya umuhimu wa lishe bora, kwa Watoto,vijana, wanawake na Wazee ili kuweza kuchochea kasi na malengo ambayo wanataka kuyafikia kama wadau wa lishe.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akiwa ameambata na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dk.Doroth Gwajima (Mwenye Skafu) pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dk.Germana Leyna (watatu Kulia) wakiangalia mfano wa mlo kamili kutoka kwenye makundi matano ya Chakula uliopikwa na maafisa Lishe na wahudumu wa afya ngazi ya Wilaya wakati wa uzinduzi wa Siku ya lishe Kitaifa, iliyofanyika Jijini Dodoma.

Katika Maadhimisho hayo pia Dkt. Germana amemuomba Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuweza kuruhusu siku ya Lishe iweze kufanyika kuanzia ngazi ya Wilaya hadi taifa kwa siku zijazo, ili kuwza kuhakikisha elimu ya lishe itakayotolewa katika siku hiyo, iweze kuwafikia watanzania wengi Zaidi.

“Uwepo wa sikukuu hii utatoa fursa ya kipekee kuendelea kuifikia Jamii ya Watanzania kwa kutoa elimu sahihi ni namna gani ya kuweza kula, lakini vilevile namna ya kuweza kutekeleza kwa umahiri afua mbalimbali za lishe ambazo zinaendelea hapa nchini”Alisema Dkt. Germana.

Mwakilishi wa  Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambaye pia ni Mkuu wa wilaya ya Chemba Simon Odunga akiteta jambo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati wa uzinduzi wa siku ya Lishe, maadhimisho ambayo yalifanyika Jijini Dodoma hivi karibuni.

Akitoa salamu kwa niaba ya kikundi cha Wafadhili wa Lishe, Tumaini Mikindo kutoka Jukwaa la Lishe Tanzania ameipongeza serikali kwa juhudi ambazo imeendelea kuchukua katika kuimarisha utekelezaji afua za lishe nchini, na kusaidia kupunguza matatizo ya utampiamlo na udumavu.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Afya) kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dk.Doroth Gwajima  alisema kupitia IWzara hiyo imekuwa ikitenga kiasi cha Sh.1,000 kwa kila halmashauri kwa ajili ya kuimarisha lishe ya Watoto.

Dk. Gwajima alisema fedha hizo zilianza kutengwa 2017-2018 ambapo zilipatikana Tsh. Bilioni 9 na zikatumika asilimia 30 tu,  huku mwaka 2018-2019 zilitengwa Tsh. Bilioni 15 zikatumika kwa asilimia 45.

Hata hivyo Dk. Gwajima alisema Waziri wa Nci, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Selemani Jafo amekuwa akifuatilia tangu alipopewa jukumu  hilo na Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan baada ya kusainia mikataba ya Lishe na Wakuu wa mikoa ambao walishusha kwa wakuu wa wilaya hadi katika ngazi ya Vijiji na dhamana kufuatilia akapewa waziri huyo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

MOI YATOA MAFUNZO YA CORONA KATA YA KISUKURU

MOI YATOA MAFUNZO YA CORONA KATA YA KISUKURU Taasisi ya Tiba ya Mifupa MOI imetoa mafunzo ya namna ya kujikinga na ugonjwa wa Corona kwa...