FEDHA ZA CRDB BANK MARATHON KUTUMIKIA KWENYE MATIBABU YA WATOTO WANAOTIBIWA KATIKA TAASISI YA MOYO YA JAKAYA KIKWETE

FEDHA ZA CRDB BANK MARATHON KUTUMIKIA KWENYE  MATIBABU YA WATOTO WANAOTIBIWA KATIKA TAASISI YA MOYO YA JAKAYA KIKWETE

Na, Mwandishi Wetu Dar es salaam.

Benki ya CRDB imeandaa mbio za CRDB Bank Marathon kwa ajili ya kuchangisha fedha za matibabu ya moyo kwa watoto wanaotoka katika familia zisizo na uwezo wa kuchangia gharama za matibabu wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Hassan Suluhu anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mbio hizo zitakazofanyika tarehe 16/08/2020 kuanzia saa 12 asubuhi jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa Habari uliofanyika leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema lengo la kuandaa mbio hizo ni kuleta tabasamu kwa watoto wenye matatizo ya moyo pamoja na familia zao.

Nsekela alisema licha ya kuandaa mbio hizo Benki ya CRDB imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha watoto wenye matatizo ya moyo ambao wanatoka katika familia zisizokuwa na uwezo wa kuchangia gharama za matibabu wanapata matibabu kama watoto wengine.

“Hadi sasa Benki yetu imechangia   kiasi cha shilingi milioni 100 fedha ambazo zilitumika kulipa gharama za upasuaji wa moyo kwa watoto 50”.

“Kiasi cha fedha kitakachopatikana katika mbio hizi kitaenda kulipia gharama za upasuaji wa moyo kwa watoto wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete”, alisema Nsekela.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB   Abdulmajid  Nsekela akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mbio za CRDB Bank Marathon ambazo lengo lake ni  kuchangisha fedha za matibabu ya moyo kwa watoto wanaotoka katika familia zisizo na uwezo wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).


Mkurugenzi huyo  Mtendaji alisema kila mshiriki wa mbio hizo ambazo zitafanyika Tanzania nzima mahali ambako benki hiyo ipo (Virtual Marathon)  atachangia kiasi cha shilingi 30,000/= na kutakuwa na mbio za kilomita 5, 10 na 21 pamoja na mbio za baiskeli.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi aliipongeza Benki ya CRDB kwa kutambua haki ya mtoto ya kupata matibabu na kuamua kuwasaidia watoto wanaosumbuliwa na magonjwa ya moyo wanaotibiwa JKCI

Prof. Janabi alisema asilimia kubwa ya watoto wanaotibiwa katika Taasisi hiyo wanasumbuliwa na magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni matundu na mishipa ya damu ya moyo kutokuwa katika mfumo  wa kawaida.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akizungumza kuhusu asilimia kubwa ya watoto wanaotibiwa katika Taasisi hiyo kusumbuliwa na  magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo wakati wa mkutano wa waandishi wa habari  uliofanyika leo jijini Dar es Salaam uliohusu mbio za CRDB Bank Marathon.

Naye Meneja wa kanda ya Mashariki wa mpango wa Taifa wa damu salama Dkt. Kokuhabwa Mkurasi aliwaomba wananchi wenye afya njema kujitokeza kwa wingi kuchangia damu siku hiyo ya CRDB Bank Marathon.

Dkt. Kokuhabwa alisema wataalamu kutoka katika ofisi yake watakuwepo kuanzia asubuhi hadi mwisho wa mbio hizo ili wananchi waweze kuchangia damu kwani wanahitaji damu za kutosha.

Sambamba na mbio hizo ambazo zitafanyika katika uwanja wa Farasi  Osterbay jijini Dar es  Salaam kutakuwepo na huduma za ushauri na upimaji wa magonjwa ya moyo, homa ya ini pamoja na uchangiaji wa damu.

 

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MATOKEO YA UTAFITI WA HALI YA LISHE YA WANAFUNZI SHULE YA MSINGI YATOLEWA

TFNC YAIBUKA MSHINDI WA JUMLA MAONESHO YA SIKU YA CHAKULA DUNIANI.

WANAFUNZI WANYWE MAZIWA SHULENI-UMMY MWALIMU.