HOSPITALI YA MIREMBE YABORESHA UTOAJI WA HUDUMA ZA AFYA
HOSPITALI YA MIREMBE YABORESHA UTOAJI WA HUDUMA ZA AFYA.
Na, Mwandishi wetu
Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe imefanya mabadiliko katika utoaji wa huduma za matibabu kwa wagonjwa wa nje, ambapo muda wa kuanza kutoa matibabu ni saa moja asubuhi badala ya saa mbili asubuhi.
Lengo la uongozi wa hospitali kufanya mabadiliko hayo ni kuboresha huduma za afya ili kuwezesha watu mbalimbali kupata huduma za matibabu mapema zaidi na kwa wakati.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, Dkt. Paul Lawala
amesema mabadiliko hayo yanahusu huduma zote za afya; ikiwamo huduma za afya ya
akili pamoja na magonjwa ya mwili.
Dkt. Lawala amesema tangu kuanza kwa utekelezaji wa mabadiliko hayo kumekuwapo na matokeo chanya kwa kuwa watumishi wamefurahia kuanza kutoa huduma mapema, huku wagonjwa na ndugu wakifurahia utaratibu mpya wa kupatiwa huduma mapema na kurejea nyumbani mapema.
“Matokeo chanya yameanza kuonekana kwani watumishi wameitikia wito wa kuwahi mapema na kuanza kutoa huduma saa moja asubuhi.
Hatua hii imesaidia watu mbalimbali kupata huduma za matibabu mapema na kwa wakati na pia watu wengi wamevutiwa na mabadiliko haya,” amesema Dkt. Lawala.
Naye Mkuu wa Kitengo Cha Wagonjwa wa Nje, Dkt. Isack Mrimi amewataka wananchi kufika katika hospitali hiyo kupata huduma za matibabu kwa kuwa Mirembe ina wataalamu wabobezi wenye uwezo wa kutoa huduma bora na kwa wakati.
Huduma za afya katika Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe zinatolewa na wataalamu wetu ambao wako tayari kukuhudumia wakati wote.
Maoni
Chapisha Maoni