WAZIRI UMMY AMESEMA UGONJWA WA KIFUA KIKUU UNAENDELEA KUPUNGUA NCHINI

WAZIRI UMMY AMESEMA UGONJWA WA KIFUA KIKUU UNAENDELEA KUPUNGUA NCHINI

Na WAJMW-Dodoma

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema maambukizi ya Kifua Kikuu (TB) yamepungua nchini kutoka wagonjwa  164,000 mwaka 2015 hadi kufikia wagonjwa 142,000 mwaka 2018.

Waziri Ummy amesema hayo leo wakati akikabidhi Hadubini 57 katika Mkoa wa Dodoma zitakazotumika kufanya vipimo vya ugonjwa wa Kifua Kikuu ambazo zitasambazwa katika Hospitali na Vituo vya Afya mbalimbali mkoani humo.

“Leo nimeanza zoezi la kukabidhi Hadubini 941 zilizonunuliwa na Serikali kwa ufadhili ya Global Fund zenye thamani ya Tsh. Bilioni 3.3 ambapo leo nitamkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Binilith Mahenge Hadubini 7 za Wilaya ya Chamwino zitakazosambazwa katika vituo vya Afya mbalimbali”. Amesema Waziri Ummy.


Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya Hadubini 7 za kuchunguza kifua kikuu zilizotolewa na Wizara kwa Wilaya ya Chamwino.

Pamoja na hayo Waziri Ummy ametumia muda huo kueleza mafanikio yaliyofikiwa na Mpango wa Taifa wa Kifua Kikuu na Ukoma ikiwa ni pamoja na kupungua maambukizi mapya kwa asilimia 18 lengo likiwa ni asilimia 20 na vifo vimepungua kwa asilimia 27 lengo likiwa ni asilimia 35.

Aidha, Waziri Ummy amesema ugunduzi wa Kifua Kikuu unaendelea kuimarika ambapo idadi ya wagonjwa waliogundulika na kuwekwa kwenye matibabu imeongezeka kutoka wagonjwa 62,180 mwaka 2015 hadi kufikia 82,,140 mwaka 2019.

Kwa upande wa vituo vya ugunduzi wa tiba, Waziri Ummy amesema katika kipindi cha miaka mitatu vituo vimeongezeka kutoka 662 mwaka 2016 hadi kufikia vituo 1201 mwaka 2019.

Katika kipindi cha miaka idadi ya wagonjwa waliogundulika kuwa na Kifua Kikuu imepungua kutoka wagonjwa 164,000 mwaka 2015 hadi 142,000 mwaka 2018.


Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu akikabidhi moja ya Hadubini za kuchunguza ugonjwa wa kifua kikuu kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Bilinith Mahenge, Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Mhe. Vumilia Nyamaga, Mbunge wa Chilonwa Mhe. Joel Mwaka huku Mkurugenzi wa huduma za kinga Dkt. Leonard Subi akishuhudia.

Waziri Ummy amesema vifo vinavyotokana na TB vimepungua  kutoka makadirio ya vifo 30,000 mwaka 2015 hadi vifo 22,000 mwaka 2018.

Waziri Ummy ameongeza kuwa Hadubini hizo zitapelekwa katika vituo vipya vya kutolea Huduma za afya 487 ambavyo vimejengwa, Hospitali za Mikoa 3, Hospitali za Wilaya 69 pamoja na vituo vya afya vya zamani 315 pia kubadilisha hadubini zilizoharibika katika vile vituo vyenye uhitaji.






Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MATOKEO YA UTAFITI WA HALI YA LISHE YA WANAFUNZI SHULE YA MSINGI YATOLEWA

TUMIENI TAALUMA ZENU KUTATUA CHANGAMOTO ZA MASUALA YA CHAKULA NA LISHE KWENYE JAMII.

TFNC YAIBUKA MSHINDI WA JUMLA MAONESHO YA SIKU YA CHAKULA DUNIANI.