SERIKALI YATOA RIPOTI YA UCHUNGUZI WA MAABARA YA TAIFA YA AFYA YA JAMII NA KUBAINI MAPUNGUFU MBALIMBALI
SERIKALI YATOA RIPOTI YA
UCHUNGUZI WA MAABARA YA TAIFA YA AFYA YA JAMII NA KUBAINI MAPUNGUFU MBALIMBALI
Na WAMJW – Dar es Salaam
23/05/2020
Serikali imetoa ripoti ya uchunguzi wa Maabara ya
Taifa ya Afya ya Jamii iliyoko ofisi za Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa
ya Binaadam (NIMR) jijini Dar es Salaam na kubaini mapungufu mbalimbali ya
kiutendaji yaliyokuwepo katika maabara hiyo.
Akiwasilisha taarifa ya
kamati hiyo leo jijini Dar es Salaam, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, Mheshimiwa Ummy Mwalimu ametaja mapungufu
yaliyobainishwa na kamati hiyo kuwa moja kati ya mashine za kupima
sampuli za COVID-19 ilikuwa na hitilafu bila uongozi wa maabara kuchukua hatua
za kuifanyia matengenezo.
Taarifa hiyo pia imebaini
kuwepo kwa upungufu katika mfumo wa kimuundo, kiutendaji na
uendeshaji wa kitaaluma katika upimaji wa vipimo, uhakiki wa ubora wa majibu na
udhaifu katika uhifadhi wa vipimo vya COVID-19.
Waziri Ummy amesema kamati hiyo pia imetaja kuwepo kwa
upungufu wa wataalamu wenye sifa za mafunzo ya “Biotechnology & molecular
Biology” katika sekta ya Afya ikiwemo katika Maabara Kuu ya Taifa.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu, akizungumza na waandishi wa Habari (Hawapo Pichani) kuhusu matokeo ya uchunguzi wa kamati iliyoundwa kuchunguza maabara ya Afya ya Jamii iliyopo NIMR jijini Dar es salaam, kufuatia kutoa majibu yenye mkanganyiko ya Vipimo vya ugonjwa Corona.
Kufuatia taarifa ya kamati ya uchunguzi wa Maabara
ya Taifa kuhusu upimaji wa sampuli za ugonjwa wa COVID- 19, Wizara ya Afya imechukua
hatua ya kuhamisha shughuli za upimaji wa COVID – 19 kutoka kwenye maabara
iliyoko NIMR na kuanza kutumika kwa
mashine nyingine za maabara mpya iliyopo Mabibo, Dar es salaam.
“Kuanzia sasa shughuli zote za upimaji wa maabara ya taifa zitafanyika
katika maabara mpya ya mabibo yenye vifaa vya kisasa vyenye ubora na uwezo wa
kupima sampuli 1,800 ndani ya masaa 24” amesisitiza Waziri Ummy.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu, akizungumza na madereva wa malori yanayoenda nje ya nchi, namna ya kuchukuliwa vipimo vya maambukizi ya ugonjwa wa Corona, baada ya kufika katika maabara za afya ya jamii zilizopo Mabibo, kwa ajili ya kuchukuliwa vipimo.
Amesema maabara iliyokuwa inatumika awali na kukutwa na mapungufu ilikuwa na uwezo wa kupima sampuli 300 kwa masaa 24 na ilianzishwa mwaka 1968 katika ofisi za Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binaadam (NIMR), mtaa wa Obama kati kati ya jiji la Dar es Salaam zitaendelea kupima magonjwa mengine.
“hivi sasa Upimaji wa Sampuli zote za COVID-19 umehamishiwa kwenye
Maabara hii ya Mabibo, Dar es Salaam ambayo kuanzia sasa ndiyo itakuwa Maabara
ya Taifa ya Afya ya Jamii. Maabara hii ambayo ujenzi wake umekamilika mwezi huu
ina miundombinu inayojitosheleza, mashine za kisasa zinazoweza kupima sampuli
nyingi na kutoa majibu ya uhakika na kwa haraka” amesema Waziri Ummy.
Aidha, Wizara imeshaandaa wataalam zaidi wenye sifa na vigezo kwa ajili
ya Maabara hiyo na imeanza kurekebisha mfumo wa utawala, utendaji na kitaaluma
ndani ya Maabara ya Taifa
Jengo
la Maabara mpya ya Afya ya Jamii iliyopo Mabibo jijini Dar es salaam,
ambayo itatumika rasmi kuchukua vipimo vya wahisiwa wa ugonjwa wa
virusi vya Corona nchini.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel
Makubi ametoa mwongozo wa kusaidia jamii kushiriki katika ibada ya shukrani na
sala ya Eid El Fitr kwa hali ya usalama ili kuepusha kuongezeka kwa maambukizi
ya virusi vya corona.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Prof. Makubi
amewataka wananchi kuchukua tahadhari
katika siku tatu ambazo nchi itaingia katika maombi maalum ya kumshukuru
Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kupungua kwa maambukizi ya virusi ugonjwa wa
Corona.
“ ni muhimu wananchi wakasherehekea salama kwa
kuchukuwa tahadhari kwani ugonjwa huo
bado upo” Amesisitiza Mganga Mkuu wa Serikali.
Katika kufanikisha uwepo
wa mazingira salama wakati wa shukrani na sala ,Viongozi wa Mitaa, Viongozi wa
Afya na uongozi wa maeneo yote ya Ibada na misikitini wanapaswa kuhakikisha
uwepo wa vifaa vya kunawia mikono, maji tiririka na sabuni au vitakasa mikono
kwa ajili ya usafi binafsi wa waumini wote katika maeneo ya kuingilia .
Aidha, Prof. Makubi
ameshauri sehemu za kufanyia ibada ziwe na nafasi ya viti kupangwa zaidi ya
mita moja kwa wale wanaokaa au kusimama na wananchi wote wanapokwenda kushiriki
au kutembelea maeneo ya Ibada/Sala wanashauriwa watumie barakoa za vitambaa
ambazo kwa sasa zipo kwa wingi na zinatengenezwa hapa nchini na wananchi
wenyewe.
Amewataka wananchi
kuepuka mikusanyiko na kuhakikisha wanakaa umbali usipoungua mita moja kati ya
mtu na mtu wakati wote wa shukrani na wakati wa shukrani waendesha ibada/sala
wawakumbushe wananchi mara kwa mara kuzingatia taratibu za kujikinga na
maambukizi kama inavyoelekezwa na wataalamu wa afya.
Mganga Mkuu wa Serikali
amewakumbusha Wamiliki wa vyombo vya usafiri wa umma kuzingatia maagizo ya
Serikali ya kutosimamisha abiria kwenye mabasi, na vilevile wahudumu wote wawe
wamevaa barakoa za vitambaa.
Maoni
Chapisha Maoni