SERIKALI INAHAKIKISHA WALENGWA WOTE WA CHANJO WANAFIKIWA KATIKA KIPINDI CHA CORONA

SERIKALI INAHAKIKISHA WALENGWA WOTE WA CHANJO WANAFIKIWA KATIKA KIPINDI CHA CORONA

Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia Mpango wa Taifa wa Chanjo imejipanga kuwafikia walengwa wote waliostahili kupata chanjo na kuhakikisha kiwango kinabaki vilevile kama ilivyotarajiwa.

Hayo yamesemwa na Ofisa Mradi kutoka Mpango huo Lotalis Gadau wakati wa usimamizi elekezi wa kukagua utoaji huduma za chanjo  katika Mkoa wa Pwani  kwa kushirikiana na Engender Health kupitia Merck Sharp& Dohme B.V (MSD).

Gadau alisema kuwa katika kipindi hiki cha nchi kukabiliana na Ugonjwa wa Corona, Wizara imejipanga kuhakikisha watoa huduma wa afya wanaendelea kutoa huduma za chanjo kwa watoto wadogo pamoja na wasichana ambao walikua wapate chanjo ya kujikinga na saratani ya mlango wa kizazi(HPV).

“Kama Wizara tumejipanga vizuri kwa kuhakikisha chanjo zote zinakuwepo kwa wakati kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na kuhakikisha watoto wote waliokuwa wanatarajia kupata chanjo wanapata,na watoa huduma wanachukua tahadhari zote za kujikinga na ugonjwa huu”,

Alisema walikuwa wakisikia wananchi wana wasiwasi kufika kwenye vituo vya kutolea huduma,“tumepita kwenye vituo vya afya kwenye mkoa huu na tumeona hali ni nzuri kwani wazazi na mabinti wengi wanakuja kwenye vituo na tumewasisitiza kila mmoja anayeenda awe balozi anaporudi nyumbani kuhakikisha wataambiana ili kila anayestahili kupata chanjo anaenda kwenye kituo cha afya chochote cha jirani aweze kupata chanjo”.

Vile vile alisema kuhusu mabinti ambao waliokua wapate  chanjo ya kuzuia  saratani ya malango wa kizazi  tofauti na awali ambapo walikua wakifuatwa mashuleni inasisitizwa wafike kwenye  vituo cha kutolea huduma za afya  vya karibu waweze kupata chanjo hiyo.

 Upande wa watoto wadogo, Bi. Gadau amesema hivi sasa umewekwa utaratibu kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka miwili ambao wanastahili kupatiwa chanjo wao wanatakiwa kupata chanjo kama ilivyo kawaida”Kwa kipindi hiki watoto ambao wamekamilisha ratiba ya chanjo na wanafika kituoni kwa ajili ya uzito tu wao wanatakiwa waende kila baada ya miezi mitatu hii ni kuepuka misongamano na tunasisitiza elimu ya afya ambayo ilikua ikitolewa kwa muda mrefu au kusubiriana kwa sasa  itatolewa kwa muda mfupi usiopungua dakika tano lakini endapo mtoto atapata homa au tatizo lolote anatakiwa kupekekwa kwenye kituo cha afya kwa ajili ya matitabu.

Naye Mratibu Huduma za Chanjo kwa Mkoa wa Pwani Abbas Hincha amesema kuwa asilimia 90 ya walengwa wa chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi kwa mabinti wenye umri wa miaka 14 ambao hapo awali walikuwa wakipatiwa wakiwa shuleni ila kutokana na janga hili wanashirikia na walimu wa shule zao kwani walikua wameandikishwa hivyo wanawapatia namba za simu na kuwapigia wazazi na walezi ili kuwapeleka kupatiwa chanjo hiyo.

Alisema katika mkoa wake wamepanga mikakati mbalimbali ikiwemo ya kuwashirikisha  watoa huduma ngazi ya jamii kuwatafuta mabinti hao kwenye maeneo yao na kuwakumbusha kwenda kupata chanjo.

Alisema muamko kwa chanjo kwa upande wa watoto wadogo unaendelea vizuri na kuna muitikio mzuri hivyo wanaendela kutoa elimu jinsi ya kujikinga na Corona na kwenye vituo ambavyo havina nafasi kubwa wanatoa huduma hizo nje ya kituo ili kuzingatia umbali wa mita moja kati ya mtu na mtu

 

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MATOKEO YA UTAFITI WA HALI YA LISHE YA WANAFUNZI SHULE YA MSINGI YATOLEWA

TFNC YAIBUKA MSHINDI WA JUMLA MAONESHO YA SIKU YA CHAKULA DUNIANI.

WANAFUNZI WANYWE MAZIWA SHULENI-UMMY MWALIMU.