Jumatano, 23 Septemba 2020

WAANDISHI WA HABARI TUMIENI KALAMU ZENU KUANDIKA KWA WINGI HABARI ZA LISHE.

WAANDISHI WA HABARI TUMIENI KALAMU ZENU KUANDIKA KWA WINGI HABARI ZA LISHE.

NA MWANDISHI WETU

Wito umetolewa kwa Waandishi wa habari kutumia kalamu zao kuandika kwa wingi habari zinazohusiana na masuala ya Lishe na Afya ili kuweza kubadili mitazamo na tabia za jamii zilizopo kuhusu masuala ya Lishe na kuweza kuleta ufanisi katika kupambana na Utapiamlo na Kujenga Taifa lenye Watu wenye Afya Bora.

Hayo yamebainishwa mkoani Shinyanga na Mganga Mkuu Dkt. Yudas Ndungile wakati akifungua Semina ya Waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa Lishe katika kuimarisha Kinga Dhidi ya Magonjwa, ambayo imeratibiwa na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania kwa Kushirikiana na Shirika lisilo la Kiserikali la World Vision Tanzania.

 Dkt. Yudas amesema waandishi ni miongoni mwa wadau wakuu wa mawasiliano yanayolenga kubadili mitazamo na tabia za jamii kuhusu masuala ya Afya na Lishe hivyo mafunzo hayo yatasaidia kuwajengea uelewa mpana zaidi kuhusu masuala ya lishe hatua itakayowasaidia kuandika taarifa zenye usahihi.

“Sote tunatambua mchango wa vyombo vya habari katika kutoa taarifa, kuelimisha na pia kuburudisha, Lakini kwa miaka ya hivi karibuni dhima hiyo imepanuka na kujumuisha masuala ya ufuatiliaji, kupaza sauti za watu wasio na sauti katika jamii, kusaidia kulinda maslahi ya jamii na mambo mengine mengi, hivyo wanahabari wanaweza kuendelea kuhabarisha, kuelimisha kuhusu umuhimu wa lishe katika kuimarisha kinga dhidi ya magonjwa” alisema Dkt. Dkt. Yudas

 


Mganga Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dkt:Yudas Ndungile akizungumza na waandishi wa habari  (hawapo Pichani) wakati wa ufunguzi wa semina ya Waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa lishe katika kuimarisha kinga dhidi ya Magonjwa, ambayo imetolewa na Taasisi ya Chakula na Lishe kwa kushirikiana na World Vision Tanzania.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Elimu ya Lishe na Mafunzo wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Sikitu Kihinga alisema mafunzo hayo yanakuja katika wakati ambao Taasisi ya Chakula na Lishe imeendelea kujikita zaidi katika kushirikiana na wanahabari kwa kuhakikisha wanajengewa uwezo na kuwa wabobezi katika kuandika habari za zinazohusu masuala ya lishe


Mkurugenzi wa Elimu ya Lishe na Mafunzo wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Sikitu kihinga, akielezea  malengo ya mafunzo ambayo yametolewa kwa waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga kuhusu Umuhimu wa Lishe katika kuimarisha kinga dhidi ya Magonjwa, ambapo Taasisi hiyo pia imeshirikiana na Shirika la World Vision Tanzania

Sikitu alisema wameamua kushirikiana na shirika la World Vision Tanzania, kwani wao pia ni wadau wakubwa wanaosimamia suala la lishe, na wamekuwa mstari wa mbele katika kupambana na Utapiamlo na Udumavu ili kwenda sambamba Serikali katika kufkia malengo iliyojiwekea katika kupambana magonjwa hayo.

Waandishi wa habari wa mkoa wa Shinyanga waliojitokeza kushiriki semina juu ya umuhimu wa lishe katika kuimarisha kinga dhidi ya Magonjwa, wakifuatilia  mafunzo ambayo yametolewa na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania kwa kushirikiana na World Vision Tanzania 

Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania kwa kushirikiana na World Vision Tanzania mbali na kutoa mafunzo haya kwa wanahabari wa mkoa wa Shinyanga pia wanatarajia kuyafanya kwa waandishi wa habari katika mkoa wa Singida, ili kuweza kuwajengea uwezo nao katika kuandika habari zinazohusiana na masuala ya Chakula na Lishe.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

  

MOI YATOA MAFUNZO YA CORONA KATA YA KISUKURU

MOI YATOA MAFUNZO YA CORONA KATA YA KISUKURU Taasisi ya Tiba ya Mifupa MOI imetoa mafunzo ya namna ya kujikinga na ugonjwa wa Corona kwa...