Dondoo za Lishe

 

LISHE NA MAAMBUKIZI YA VIRUSI VYA CORONA

UJUMBE KWA JAMII

1.      Uhusiano kati ya Lishe na maambukizi ya virusi vya Corona.

Mtu mwenye hali nzuri ya lishe na mwenye hali duni ya lishe wote wana nafasi sawa ya kuambukizwa virusi vya Corona. Ugonjwa wa Corona utokanao na virusi vya Corona, Kama ilivyo Kwa magonjwa mengine ya kuambukiza kuwa una uhusiano mkubwa na hali ya lishe ya mtu aliyepata maambukizi hayo. Tofauti ni kwamba mtu mwenye hali nzuri ya lishe huwa na kinga mwili imara hivyo huweza kuwa na uwezo mkubwa wa kupambana na maambukizi, ikilinganishwa na yule mwenye hali duni ya lishe na kinga mwili dhaifu. Hii ina maana kuwa virusi hivi husababisha athari zaidi kwa watu wenye kinga mwili dhaifu.

Maambukizi ya virusi vya Corona huambatana na dalili mbalimbali. Dalili kuu ya maambukizi haya ni kupata homa kali pamoja na mafua, kikohozi kikavu na kupumua kwa shida. Uwepo wa maambukizi haya hubadili utendaji kazi wa mifumo mbalimbali ya mwili, kwani  mwili hulazimika kufanya kazi ya ziada katika kukabiliana nayo; Hali inayoambatana na kuharibika kwa seli na tishu mbalimbali za mwili. 

Mabadiliko hayo ya mwili pia husababisha kujitokeza kwa matatizo mbalimbali, yakiwemo kukosa hamu ya kula, kichefuchefu, kutapika, umeng’enyaji duni wa chakula na usharabu (ufyonzwaji) duni wa virutubishi. Hali hizo hupelekea mlengwa kushindwa kula chakula cha kutosha kukidhi mahitaji ya kilishe, hivyo kuongeza tatizo la uhitaji wa virutubishi mwilini.

Aidha uwepo wa homa na matatizo mengine yanayoambatana na maaambukizi ya virusi vya Corona husababisha upotevu wa maji mwilini ambayo ni muhimu katika kukamilisha utendaji wa shughuli mbalimbali za mwili. Upotevu wa maji huambatana na kupotea kwa viasili vinavyohusika na uimalishaji  kinga mwili kama protini na baadhi ya madini na  vitamini. Hivyo Kuufanya mwili kuwa dhaifu kutokana na kupungua kwa virutubishi na kingamwili ya kupambana na athari za maambukizi.

Athari za maambukizi kwa watu hutofautiana kutokana na mambo yafuatayo:

Hali ya lishe: Uwezo wa mwili kupambana na maambukizi ya virusi vya Corona unategemea hali ya afya na lishe ya mtu husika. Mtu mwenye Afya na lishe bora mwili wake unakuwa na uwezo mkubwa wa kupambana na maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Corona. Hali nzuri ya lishe huimarisha kinga ya mwili na kumsaidia muathirika kupambana na virusi vya ugonjwa wa Corona na hivyo kupata athari kwa kiasi kidogo. Mtu mwenye hali duni ya lishe huwa na kinga mwili dhaifu hivyo apatapo maambukizi ya virusi vya Corona mwili wake huwa na uwezo mdogo wa kupambana hali inayosababisha kupata madhara makubwa, kuchelewa kupona na kwa baadhi ya watu kupoteza maisha.

Homa: Uwepo wa homa huchangia hali ya mgonjwa kuwa mbaya zaidi ikilinganishwa na mgonjwa asiyekuwa na homa. Homa huambatana na kukosa hamu ya kula na kupotea kwa maji mwilini na kuufanya mwili kuwa dhaifu hivyo kuongeza athari kwa mlengwa.

Magonjwa mengine: Uwepo wa magonjwa mengine mfano magonjwa sugu yasiyoambukiza kama vile kisukari,  kifua kikuu, UKIMWI, saratani, shinikizo la juu la damu na magonjwa mengine ya moyo huchangia hali ya mlengwa kuwa mbaya ikilingwanishwa na  yule asiyekuwa na ugonjwa  kwa sababu uwepo magonjwa hayo huchangia katika kupunguza kinga mwili.

Umri wa mlengwa: Watu wenye umri mkubwa (wazee) hupata athari kubwa wanapokuwa na maambukizi kwa sababu ya udhaifu wa mifumo mbalimbali ya miili yao pamoja na ulaji duni  hali inayowafanya washindwe kukidhi mahitaji ya kilishe  na kupungua kingamwili. Kundi hili lipatapo maambukizi ya virusi vya Corona athari huwa kubwa zaidi.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

MOI YATOA MAFUNZO YA CORONA KATA YA KISUKURU

MOI YATOA MAFUNZO YA CORONA KATA YA KISUKURU Taasisi ya Tiba ya Mifupa MOI imetoa mafunzo ya namna ya kujikinga na ugonjwa wa Corona kwa...